Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, amewataka viongozi waSerikali za Mitaa nchini kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kufungua rasmi Mkutano Mkuu wa 39 wa ALAT jijini Dodoma tarehe 11 Machi, 2025, Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana kwa maneno pekee bali kwa vitendo, akiwataka viongozi wa Serikali za Mitaa kutumia rasilimali za umma kwa uwajibikaji mkubwa na kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.
Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. SamiaSuluhu Hassan, imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha Serikali za Mitaa ili kuhakikisha maendeleo yanaanzia ngazi za chini. "Maendeleo si ahadi, ni hatua tunazochukua kila siku," amesema Waziri Mchengerwa, akinukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere: "Maendeleo ni kazi, si bahati. Taifa lisilo na nidhamu ya kazi haliwezi kupiga hatua."
Amesisitiza kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa ipasavyo na wananchi wanapata huduma bora, hususan katika sekta za elimu, afya,miundombinu na uchumi wa wananchi.
Ametaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa hatua zimechukuliwa kuimarisha huduma za jamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Miongoni mwa hatua hizo ni ujenzi wa madarasa na kuimarisha elimu bure ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata nafasi ya kusoma, pamoja na ujenzi wa hospitali na vituo vya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Aidha,Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu kwa ujenzi wa barabara kupitia TARURA, hatua inayounganisha vijiji na miji na kuwezesha usafirishaji wa mazao na bidhaa za biashara. Pia, Serikali imeimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, hatua inayoongeza uwezo wa halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za taifa.
Waziri Mchengerwa amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa kuwa mfano wa uwajibikaji na kushirikiana na wananchi katika mchakato wa maendeleo. Alinukuu maneno ya John F. Kennedy: "Usiulize nchi yako inaweza kukufanyia nini, bali jiulize unaweza kuifanyia nini nchi yako,"akisisitiza kuwa maendeleo ni jukumu la pamoja baina ya Serikali na wananchi.
"Hakuna maendeleo ya kweli bila ushirikishwaji wa jamii," amesema Waziri Mchengerwa, akinukuu maneno ya Nelson Mandela, na kusisitiza kuwa Serikali za Mitaa zina nafasi muhimu katika kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Waziri Mchengerwa amehitimisha kwa kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha Serikali za Mitaa zinaendelea kuwa kiungo muhimu cha maendeleo. "Tunajenga nchi kwa vitendo, si kwamaneno," amesisitiza.
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.