Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameziagiza halmashauri zote nchini kusimama imara na kuwa makini katika ukusanyaji wa mapato pamoja na matumizi yake ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa njia sahihi.
Akifungua Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma, Rais Samia amewaonya viongozi wa halmashauri dhidi ya ubadhirifu wa fedha za serikali, akimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mhe.Mohamed Mchengerwa, kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha na kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wanaoiba au kughushi risiti za mapato.
“Kama mmewabaini hawa watu walioghushi risiti, tafadhali sana, lile jicho lenu la huruma hapa hapana,” ameonya Rais Samia, akisisitiza kuwa viongozi watakaoshindwa kuwachukulia hatua wahusika watawajibishwa wao wenyewe.
Pia amekemea vikali urasimu unaokwamisha wawekezaji, akiwataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji yanatumika kama ilivyokusudiwa.
“Hakuna sababu kwa wawekezaji kusumbuliwa kwa sababu serikali inatumia nguvu kubwa kuwavutia kuja nchini kwa maendeleo ya taifa letu,” amesema Rais Samia, huku akilaani tabia ya baadhi ya viongozi wa halmashauri kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa wawekezaji wa ndani.
Amezitaka halmashauri kutumia utawala wa sheria katika kushughulikia wawekezaji wanaokiuka makubaliano ya uwekezaji ili kuepusha hasara kwa serikali. Pia alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kushughulikia migogoro ya uwekezaji.
Ameagiza halmashauri kuhakikisha kuwa mipango yao inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Pia aliwataka viongozi wenye nia ya kugombea nafasi za kisiasa katika Uchaguzi Mkuu ujao kutoa taarifa mapema ili serikali iweze kupanga mbadala wao.
“Kiongozi yeyote anayepanga kugombea ahakikishe anatoa taarifa mapema. Wale watakaogombea bila taarifa na wasifanikiwe, watajiondoa wenyewe kwenye utumishi,”amesema Rais Samia.
Katika hatua nyingine,amezipongeza halmashauri za Ludewa, Tanganyika, na Kwimba kwa matumizi bora ya mapato na ubunifu wao katika kuboresha huduma kwawananchi. Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kote nchini kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki bila usumbufu.
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.