Na Mathew Kwembe, Dodoma
Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ALAT imesema kuwa inatarajia kumtangaza Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri itakayofanya vizuri katika hafla ya utoaji wa tuzo hiyo kwa mwaka huu itakayofanyika tarehe 20 juni, 2019 huko jijini Mwanza.
Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT Taifa bwana Abdallah Ngodu alieleza jana kuwa lengo ni kuzipongeza halmashauri zilizofanya vizuri lakini pia kuzibaini halmashauri zilizofanya vibaya ili kuangalia namna ya kuzisaidia halmashauri hizo ili nazo zifanye vizuri.
Alisema kuwa ALAT itaangalia njia mbalimbali ya kuzisaidia halmashauri zitakazobainika kufanya vibaya ikiwemo kuzijengea uwezo kwa njia ya mafunzo ili nazo ziweze kufanya vizuri miaka ijayo.
“Kwa halmashauri ambazo hazifanyi vizuri tutazibainisha na tutataka kujua kwa nini hazifanyi vizuri na tukishajua sababu tuweze kutengeneza afua za kuzinyanyua hizi halmashauri ambazo hazifanyi vizuri ili nazo zifanye vizuri,” alisema
Aliongeza kuwa halmashauri zitapimwa kwa vigezo mbalimbali mathalani kama halmashauri ili kuwa imelenga kukusanya kiasi cha bilioni nne badala yake ikakusanya bilioni moja tutataka kujua kwa nini haikuweza kufikia malengo yake.
“Sisi ALAT tutatumia kigezo cha kufikia malengo ya halmashauri na ndiyo suala ambalo mara kwa mara limekuwa likisisitizwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kwa nini malengo hayakufikiwa, kwa hiyo tunaangalia tatizo ni nini? Ni uongozi au ukosefu wa ubunifu,” alisema na kuongeza:
“Tuzo ya viongozi wa serikali za Mitaa inaangalia pia namna halmashauri zilivyo na ubunifu katika utoaji wa huduma kwa wananchi na ukusanyaji wa mapato,” alisisitiza bwana Ngodu.
Alisema ALAT kwa kushirikiana na wadau wakishabaini tatizo uangalia namna ya kulitatua, mathalani kama tatizo ni mafunzo huangalia namna ya kutoa mafunzo kwa viongozi ili kuwajengea uwezo na kama tatizo ni uongozi kama kuna uwezo wa kubadilisha mfano watendaji wataishauri serikali ifanye hivyo lakini kwa upande wa viongozi wa kisiasa kama madiwani wataona namna ya kuwapa mafunzo.
Bwana Ngodu alisema ALAT inataka halmashauri zote 185 nchini ziwe na uwezo wa kujiendesha zenyewe kimapato badala ya kutegemea kwa zaidi ya asilimia 90 mapato ya serikali kuu.
Aliongeza kuwa lazima kiwango cha chini kilichowekwa kwa halmashauri kifikiwe ndiyo malengo makuu ya tuzo hii.
Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa tuzo hizo kutolewa kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2015 wakati tuzo hizo zilipoanza kutolewa ambapo mshindi alikuwa Manispaa ya Kinondoni.
Mara ya pili tuzo hizo zilitolewa mwaka 2016 ambapo tuzo hiyo ilichukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, iliyopo mkoa wa Shinyanga.
“Mwaka huu itakuwa ni mara ya tatu kuitoa tuzo hiyo ambapo halmashauri itakayoibuka mshindi wa jumla tutaizawadia tuzo hiyo,” alisema
Aliongeza kuwa mbali na halmashauri itakayoshinda tuzo ya jumla pia kutakuwa na zawadi kwa makundi manne ya halmashauri za Majiji, Manispaa, Halmashauri za Miji na Halmashauri za Wilaya
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.