Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini wamehimizwa kuitumia Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kutatua mivutano na migongano inayojitokeza baina ya Wakurugenzi wa halmashauri na Wenyeviti na Mameya wa halmashauri ili mivutano hiyo isije kuathiri ustawi wa halmashauri hizo.
Wito huo umetolewa tarehe 23 Aprili, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar.
Amesema kwa kuwa ALAT ni chombo muhimu na pekee kinachowakutanisha watendaji wa halmashauri na waheshimiwa Madiwani, hivyo kama kuna matatizo madogo madogo yanayojitokeza amewataka Viongozi hao kukitumia chombo hicho ili kuondoa migongano inayoweza kuathiri ustawi wa halmashauri.
“Kumekuwepo na mivutano na migongano kati ya wakurugenzi na madiwani, sote tunajenga nyumba moja tunavutana nini huko?” amehoji Mhe. Mchengerwa na kuongeza:
“kila mara mnawaazimia wakurugenzi, kama kuna matatizo madogo madogo, tumieni chombo chetu cha ALAT ili kuweza kuleta suluhu na kuwasaidia watanzania katika maeneo yetu.”
Amesisitiza: “pale ambapo mnaona pana hitilafu tumieni ALAT, fikisheni malalamiko yenu kule, pelekeni maoni na mimi na Mwenyekiti wa ALAT tunazungumza mara kwa mara, na mara ya mwisho tulipokutana na kamati tendaji tumezungumza kwa kina na baadhi ya mambo tumeanza kuyafanyia kazi.”
Kuhusu ukusanyaji mapato Waziri Mchengerwa amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha risiti zinatolewa kwa kila muamala ili kuzuia upotevu wa mapato.
Aidha Waziri Mchengerwa amesema kuanzia mwaka ujao wa fedha kigezo cha ziada cha kuzipima Halmashauri zote nchini ni kwa kila Halmashauri inapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato kuanzia viwili na kuendelea kwa kila mwaka wa fedha.
Mambo mengine aliyosisitiza Mhe. Waziri kuwa ni pamoja na Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa wanasikiliza kwa makini kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, na wasisubiri viongozi wa ngazi ya kitaifa watembelee halmashauri hizo ndipo wazipatie ufumbuzi kero zao.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa Mhe. Sima Constantine Sima amemweleza Mhe Mchengerwa changamoto mbalimbali zinazozikabili Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo changamoto ya umbali kutoka baadhi ya halmashauri kwenda katika bohari za serikali kwa ajili ya kuweka mafuta jambo linalosababisha magari ya serikali kutembea umbali mrefu kufuata mafuta katika bohari hizo.
Mkutano huo unaotarajiwa kukamilika tarehe 25 Aprili, 2024 unawakutanisha washiriki 600, wakiwemo Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa, Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, na Wakurugenzi wa Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na Viongozi wengine wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Jambo Letu; Shiriki kwa Maendeleo ya Taifa”
Rais wa Zanzibar Mhe.Dkt Hussein Mwinyi anatarajia kufunga Mkutano huo tarehe 25 Aprili, 2024.
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.