Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Dkt Mpango amesema ni lazima watendaji na viongozi wote wa kisiasa kufanya kazi kwa pamoja na kufanya mazungumzo ya kujenga kwa manufaa ya wananchi panapotokea hoja au mitazamo tofauti katika utekelezaji.
Makamu wa Rais ambaye katika mkutano huo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwataka viongozi hao kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo kukuza migogoro baina yao.
Dkt. Mpango amewahimiza viongozi hao kudumisha ushirikiano baina ya Madiwani na Wakurugenzi wa Halmashauri na kuondokana na tabia ya Madiwani kutoa maazimio dhidi ya Wakurugenzi pamoja Wakurugenzi kutowaheshimu Madiwani.
Pia Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa Mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato katika maeneo yao.
Ametaja tathmini ya taarifa za mapato kutoka katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vingine vilivyokusanywa kupitia mashine za POS imebaini katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa fedha hazipelekwi katika akaunti husika za benki hivyo amewasihi kuzingatia taratibu za fedha na kudhibiti matumizi yasiyo na tija.
Aidha amewahimiza Madiwani kusimamia vema Halmashauri zao na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato.
Makamu wa Rais amemtaka Waziri wa TAMISEMI kuwachukulia hatua mara moja Viongozi na Watumishi wanaobainika kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma, vitendo ambavyo husababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa kiwango cha chini kwa kuwa fedha zilizopangwa kwenda kwenye mradi husika huenda kwenye mifuko ya viongozi na watumishi wasio waaminifu.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia utawala bora, kukomesha unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, usimamizi wa Nidhamu, Maadili na Uwajibikaji pamoja na kushirikiana na jamii katika kutoa elimu na kulinda maadili ya vijana.
Pia ameagiza kuimarisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na usafi ili kuwa na maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angellah Kairuki amewahimiza viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vema Halmashauri pamoja na kuwahamasisha na kuwasimamia wananchi katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo.
Pia amesema Wizara itaendelea kushirikiana vema na ALAT katika kuzisaidia Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuweka msukumo kwa Halmashauri 56 ambazo hazijafikia makusanyo ya shilingi bilioni 2 au zaidi kwa mwaka ili ziweze kuongeza mapato.
Pia amezishauri Halmashauri kuwa chachu na tija katika kupokea wawekezaji na wafanyabiashara katika maeneo yao ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara bila vikwazo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Constantine Sima amesema Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa imefanikiwa kuziunganisha na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwezesha kupungua kwa hati chafu za ukaguzi.
Ameongeza kwamba Jumuiya hiyo inasisitiza Halmashauri zote kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha thamani halisi ya fedha inaonekana katika miradi inayotekelezwa.
Amesema mkutano huo ni jukwaa la kubadilisha uzoefu, maarifa na mifano bora katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa.
Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) inasema “Miundombinu iliyoboreshwa ni chachu ya utoaji wa huduma bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa”.
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.