Na Atley Kuni, DODOMA
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), imeipongeza Serikali kwa hatua yake ya kurejesha shughuli ya kukusanya kodi ya majengo, ushuru wa Mabango na vitambulisho vya wajasiriamali kwa Halmashauri kwani hatua hiyo itaongeza mapato kwa Serikali kwani mamlaka hizo zina mtandao mpana wa kuvifikia vyanzo hivyo vya mapato.
Akizungumza Ofisini kwake leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Bw. Moses Kaaya, amesema Jumuiya hiyo imefarijika sana kwa uamuzi huu wa Serikali kwani suala la kutaka vyanzo hivyo virejeshwe Halmashauri ilikuwa moja ya ajenda katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo, uliofanyika mwaka juzi, jijini Mwanza.
“ Katika Mkutano Mkuu wa ALAT, uliofanyika kuanzia tarehe, 22 hadi 24, Julai, 2019, jijini Mwanza, moja ya ajenda ilikuwa kutazamwa upya kwa vyanzo vya mapato na kuvirejesha katika Mamalaka ya Serikali za Mitaa, hivyo kwa hatua hii, Jumuiya ya Serikali za Mitaa tumefarijika sana,” amesema Kaaya.
Ameongeza kuwa kutokana na mtandao wa Mamlaka za Serikali za Mitaa jinsi ulivyo, unaruhusu mamlaka hizo kutambua bango gani liko wapi, hivyo ni rahisi kwa watendaji wake kuweza kukusanya ushuru wake.
“Tunaposema Halmashauri zina mtandao mpana tunamaanisha kuwa mamlaka hizi zina uwezo wa kuwafikia wananchi wake kuanzia ngazi za wilaya, kata, vijiji au Mitaa hadi vitongoji hivyo siyo rahisi kuwepo suala la ukwepaji wa kodi, kwakuwa kwa umoja wao wanao uwezo wa kujipanga na kujua vichochoro vyote,” amesema.
Amesema Serikali ina wakusanya ushuru katika ngazi za kata, mpaka vijiji na hao wote waliwezeshwa mashine za kukusanyia mapato za POS, ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kufanikisha suala la ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuzuia mianya ya ubadhilifu.
Katibu Mkuu huyo wa ALAT Taifa amekumbusha kuwa Mwaka 2019, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, iligawa mashine mpya za kisasa 7227 kwa mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweza kusaidiana na mashine 10,100 zilizokuwepo lengo likiwa ni kuzirahisishia Mamlaka hizo kukusanya mapato yake, mbalimbali
Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya fedha, tarehe 01 Februari, ilitangaza kurejeshwa kwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kuongeza wigo wa kukusanya mapato hayo, ambayo yalikuwa yakikusanywa na Mamlaka ya mapato nchini. (TRA).
Jengo la Sokoine,Barabara ya CDA Dodoma
Postal Address: P.O.Box 2049 DODOMA
Telephone: 0262323407
Mobile: +255(0)784209840 au
Email: alat_tz@yahoo.com
Copyright ©2018 ALAT . All rights reserved.